The United Republic of Tanzania

TANZANIA INVESTMENT CENTREKituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kinashiriki kwenye maonesho ya Sabasaba 2019 ili kutoa ufafanuzi wa kujisajili na Kituo na faida za huduma zake kwa mradi. .


Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kinashiriki maonesho ya 43 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba yanayofanyika kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam kuanzia tarehe 28 Juni -tarehe 13 Julai, 2019. Kauli mbiu ya maonesho ni 'usindikaji wa mazao ya biashara kwa maendeleo endelevu ya biashara'. Kauli mbiu imelenga kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli inayohimiza uanzishaji wa viwanda vya usindikaji nchini.

 

Katika kutekeleza kauli mbiu ya maonesho ya Sabasaba 2019, Kituo kinawahamisisha wawekezaji wazawa na wageni kuanzisha miradi ya uwekezaji inayolenga kuongeza thamani mazao ya kilimo ili kuzalisha bidhaa kama vile juice, mvinyo, mafuta ya kula, unga, dawa, maziwa, chakula cha mifugo, samaki na uzalishaji wa bidhaa zinazotokana na mifugo. Kwa kuwekeza katika viwanda vya kuongeza bidhaa thamani, kutawezesha nchi kufanya biashara ndani na nje ya nchi kwa bidhaa zilizoongezwa thamani badala ya kusafirisha malighafi. Hatua hiyo itawezesha wananchi na Taifa kwa ujumla kunufaika na faida zinazotokana na uwekezaji kwenye mnyororo wa thamani katika sekta ya Kilimo.

 

Ili kuunga mkono na kufanikisha miradi ya wawekezaji itakayoanzishwa katika usindikaji, Serikali kupitia TIC inatoa vivutio vya uwekezaji vya kodi na visivyo vya kikodi kwenye mitambo, mashine na bidhaa nyingine za mtaji zinazohusiana na mradi. Bidhaa hizo ni zile zinazoagizwa kutoka nje ya nchi. Hata hivyo Wadau wazingatie kwamba vivutio vya uwekezaji hutolewa tu kwa miradi iliyosajiliwa na TIC. Lengo  ni kusaidia kupunguza gharama katika hatua za awali za utekelezaji wa miradi ya uwekezaji.

 

Tunawakumbusha wadau kwamba, TIC inasajili miradi ya uwekezaji inayomilikiwa na wazawa ikiwa na thamani ya dola za Kimarekani laki moja (100,000) na dola za Kimarekani laki tano (500,000) kwa mradi utakaomilikiwa na mgeni au ubia. Kiasi hicho cha fedha kilichotajwa pia kinaweza kuwa fedha za Kitanzania zinazolingana na fedha hizo.

 

Kipekee kabisa TIC inawakaribisha washiriki wa maonesho ya sabasaba kutoka Mikoa nchi mbalimbali (mtu binafsi, kampuni, vyama vya maendeleo na taasisi mbalimbali) kutembelea banda letu ili kupata elimu ya uwekezaji, fursa za uwekezaji, ufafanuzi wa kujisajili na TIC na namna ambavyo wanaweza kunufaika na huduma zetu kwa wawekezaji. Tunapatikana kwenye Banda la Jakaya Kikwete (JK).

 

Social Medias

Copyright ©2018 Tanzania Investment Centre.
All Rights Reserved.
Designed, Developed, and Maintained by Tanzania Investment Centre(TIC)